Na Mwandishi Wetu

Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Bagamoyo na maeneo jirani, ikiwemo ajira, biashara, usafirishaji na huduma mbalimbali zitakazochochewa na uwepo wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wanaodai fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bandari hiyo wanalipwa stahiki zao.

Nyongo amesema Bandari ya Bagamoyo ni mradi wa kimkakati utakaosaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ikiunganishwa na kongani za viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya Mkoa wa Pwani.

Alisema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Bagamoyo, ambapo alikagua miradi mbalimbali, ikiwemo eneo la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo lililopo Mbegani.

“Bandari hii inajengwa katika eneo langu la utawala. Nitashirikiana na mamlaka zinazohusika kuhakikisha wananchi wanaodai fidia wanalipwa, lakini pia nitakuwa karibu kufuatilia utekelezaji wa ujenzi ili wananchi waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na mradi huu,” alisema Nyongo.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika ujenzi wa bandari hiyo, akisema mradi huo utatoa fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Bagamoyo na maeneo mengine ndani na nje ya wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mhandisi Stephen Mbogela, alisema Serikali imekamilisha uthamini na utwaaji wa eneo lote la mradi lenye ukubwa wa hekta 887.

Alisema kati ya eneo hilo, hekta 407 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya bandari, huku hekta 480 zikitengwa kwa ajili ya maeneo ya lojistiki na usafirishaji.

Mhandisi Mbogela alisema Sh bilioni 49 tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bandari hiyo katika eneo la Mbegani.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam inakaribia kufikia ukomo wa uwezo wake wa kuhudumia shehena na meli kubwa za kisasa, hivyo Bandari ya Bagamoyo itakuwa kitovu muhimu cha ziada kitakachosaidia kupunguza muda wa meli kusubiri kutia nanga na kuhudumia shehena.

“Shehena inayohudumiwa nchini imefikia zaidi ya tani milioni 30 kwa mwaka 2026 na inatarajiwa kufikia zaidi ya tani milioni 50 ifikapo mwaka 2030, kiasi ambacho kinahitaji miundombinu mipya na thabiti,” alisema Mhandisi Mbogela.

Posted in

Leave a comment