Na Abel Mwakingwe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amemtaka mkandarasi anayejenga Kampasi ya Tanga ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kampasi hiyo jijini Tanga, akisema Serikali inatarajia jengo hilo kukamilika ifikapo Mei 2027 na kuanza kutumika.

Alisema ujenzi wa kampasi hiyo una umuhimu mkubwa kwa Serikali kwa kuwa unalenga kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini.

“Serikali haitaki majengo haya yajengwe kwa ajili ya kuonekana pekee, bali yanapaswa kukamilika na kutumika kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema.

Kikwete amepongeza uongozi wa TPSC kwa usimamizi wa mradi huo, huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuzingatia viwango vinavyohitajika ili kukamilisha mradi kwa wakati.

Alisema mkandarasi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa wakati ili kuepusha uwezekano wa kuchukuliwa hatua, ikiwemo kubadilishwa iwapo atashindwa kutimiza matakwa ya mkataba.

Kikwete alisema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa ya kuendelea na ujenzi wa majengo mengine yaliyopangwa ndani ya Kampasi ya Tanga.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, ameishukuru Serikali kwa kuupa umuhimu mradi wa ujenzi wa Kampasi ya TPSC katika Mkoa wa Tanga.

Alisema uwepo wa kampasi hiyo utaongeza fursa za elimu na mafunzo kwa wananchi, sambamba na kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Tanga.

Naye Kaimu Katibu Mkuu-Utumishi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prisca Lwangili, amemshukuru Waziri Kikwete kwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya wizara, ikiwemo maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga.

Alisema ufuatiliaji huo unasaidia kuhakikisha mipango inayowekwa na Serikali inatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kampasi hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,000.

Mabonesho alimshukuru Waziri Kikwete kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa maendeleo ya mradi huo na kuendelea kuhimiza uongozi wa chuo kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unakwenda kwa kasi inayotarajiwa.

Posted in

Leave a comment