Na Cosmas Msuha

Tume ya Madini, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), inaendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo nchini ili kuboresha ujuzi wao na kuongeza tija katika sekta ya madini na uendelezaji wa Taasisi ya Uchimbaji Mdogo wa Madini (FADev).

Akizungumza na wananchi Aprili 19, 2026 mkoani Morogoro, mwakilishi wa FADev, Bi. Rehema Mkuli, alisema mkakati wa serikali unalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwajengea uwezo wa kitaalamu na kuwahamasisha kutumia mbinu salama na zenye tija katika uchimbaji.

Alisema kupitia mradi huo unaofadhiliwa na UNDP, wachimbaji watapata mafunzo ya msingi ikiwemo uchoraji wa ramani za kijiolojia pamoja na usanifu salama na bora wa mashimo ya uchimbaji.

“Tunashukuru UNDP kwa kuwasaidia wachimbaji wadogo hususani wa madini ya ujenzi na viwanda ambao mara nyingi hawapati fursa ya kufadhiliwa kwani wafadhili wengi huelekeza nguvu kwenye sekta ya dhahabu, lakini UNDP imeonyesha njia kwa kusaidia kundi hili”, alisema Bi. Mkuli.

Kwa upande wake, mkufunzi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkoa wa Morogoro, Mjiolojia Asifiwe Ngala, alielezea umuhimu wa wachimbaji kujifunza uchoraji wa ramani za kijiolojia na  kuelewa aina mbalimbali za miamba na madini yaliyomo ndani yake ili kuboresha shughuli zao.

“Ujuzi huu utasaidia kuongeza ufanisi katika utambuzi wa rasilimali asilia, kupunguza uchimbaji wa kubahatisha ili kuongeza tija katika uzalishaji,” alisema Ngala.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Vincent Mosha kutoka Kijiji cha Kinyenze, Manispaa ya Morogoro, alisema programu hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya wachimbaji wadogo.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wachimbaji kuepuka uharibifu wa mazingira, kufanya kazi kwa ushirikiano, kuweka akiba, na kusimamia vizuri mapato yao.

“Mafunzo haya yana mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wachimbaji na familia zao pamoja na kukuza sekta ya madini kwa ujumla,” alisema Mosha.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika katika mikoa minne kati ya minane iliyofanyiwa utafiti wa maendeleo ya madini, ambayo ni Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.

Posted in

Leave a comment