Na Jastini Bukebuke, Geita

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeendelea kuimarisha usalama barabarani kwa kutoa elimu kwa madereva wa magari madogo na makubwa wanaofanya kazi katika kampuni za GGML na Capital Drilling.

Elimu hiyo ilitolewa katika eneo la Shift Change Site, Kata ya Nyalwanzaja, Tarafa ya Busanda, Wilaya ya Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza ajali na kuongeza uelewa wa madereva kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkaguzi wa Polisi, INSP Gabriel Rwehimbiza, aliwataka madereva kuhakikisha wanamiliki leseni halali za udereva na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa magari ndani ya mgodi ili kuzuia ajali na kulinda maisha yao pamoja na ya watumiaji wengine wa barabara.

Alisema madereva wanapaswa kuwa mabalozi wa usalama kwa kuwaelimisha wenzao kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Aidha, alionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya madereva watakaobainika kukiuka sheria, ikiwemo kufungiwa leseni za udereva kwa mujibu wa vifungu vya 33 na 34 vya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, Marejeo ya mwaka 2023.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa IHET, Steven Reuben, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu inayochangia kuongeza uelewa wa madereva kuhusu usalama na nidhamu ya uendeshaji wa magari ndani ya mgodi.

Reuben aliwataka madereva kuhakikisha abiria wote wanaotumia magari wanafunga mikanda ya usalama, kuzingatia viwango vya mwendo vilivyowekwa na kudumisha umbali salama wanapokuwa karibu na magari makubwa ya mgodini ili kupunguza hatari ya ajali.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeendelea kutoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani wakati wote, likisisitiza kuwa kufuata sheria ni msingi wa kulinda maisha, mali na kuhakikisha mazingira salama ya kazi na usafiri.

Posted in

Leave a comment