
Na Jastini Bukebuke, Geita
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ludete wamepatiwa elimu kuhusu majukumu ya Dawati la Jinsia na Watoto jana walipotembelea Kituo cha Polisi Katoro kilichopo Mji Mdogo wa Katoro, Wilaya ya Geita kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Jeshi la Polisi.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Geita, SP Severia Nauyo, alisema ziara hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu namna Polisi Jamii inavyotekeleza majukumu yake ya kutoa elimu kwa wananchi, kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii, pamoja na kushirikisha makundi mbalimbali katika kuzuia uhalifu na kuimarisha usalama.
SP Nauyo aliwapongeza wanafunzi hao wa Kidato cha Nne kwa kuonyesha uthubutu na utayari wa kujifunza kuhusu majukumu ya Jeshi la Polisi, hususan namna Dawati la Jinsia na Watoto linavyopokea na kushughulikia malalamiko na migogoro ya kijamii kwa kuzingatia sheria, taratibu na haki za wahusika.
Aidha, aliwahimiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wa amani kwa kutoa taarifa kwa walimu, wazazi, walezi na Jeshi la Polisi pindi wanapoona viashiria vya uhalifu, ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa watoto au vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na amani katika jamii.
Kwa upande wao, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ludete walilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu, wakieleza kuwa imewaongezea uelewa kuhusu majukumu ya Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani, usalama na utulivu.
Pia walilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi, haki na bila ubaguzi, jambo ambalo limeendelea kuimarisha imani ya jamii kwa Jeshi hilo.

Leave a comment