Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limebadilisha ratiba ya Upimaji na Mitihani ya Taifa ya mwaka 2026, ambapo mitihani na upimaji uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba umehamishiwa sehemu kubwa ya Oktoba kutokana na tahadhari ya uwezekano wa mvua kubwa za El Niño.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne sasa utafanyika Oktoba 5 na 6, badala ya Oktoba 21 na 22, 2026.

Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili, uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 17 na 18, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8.

Kwa upande mwingine, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 2 hadi 13, sasa utafanyika Oktoba 12 hadi 23.

Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kuanza Novemba 9 hadi 27, sasa utaanza Oktoba 19 na kumalizika Novemba 6, 2026.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu, Wanu Hafidh Ameir, marekebisho hayo yamefanyika kwa lengo la kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani.

Posted in

Leave a comment