Na Pilastus Nyaulingo

Takribani wafanyakazi 7,000 wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu wamepimwa afya zao, huku matumizi ya teknolojia katika shughuli za uchimbaji yakitajwa kuwa miongoni mwa hatua zinazolenga kupunguza ajali, majeraha na changamoto za kiafya kwa wafanyakazi.

Hatua hiyo imeelezwa wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea mgodi huo uliopo katika Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohusu usalama na afya mahali pa kazi.

Kamati hiyo imeitaka sekta ya madini kuendelea kuimarisha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi, pamoja na kuhakikisha wafanyakazi na wakandarasi wanapatiwa mafunzo ya kutosha kuhusu vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika shughuli za uchimbaji.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Mchafu Chakoma, alisema kamati imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika mgodi huo kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira salama.

Alisema mafunzo ya usalama yanapaswa kuendelea kutolewa kwa wafanyakazi na wakandarasi ili waweze kutambua vihatarishi na kuchukua tahadhari wanapotekeleza majukumu yao.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, alisema mgodi huo umetenga na kutumia takribani Sh bilioni mbili kila mwaka kupitia programu za uwajibikaji kwa jamii (CSR).

Kwa mujibu wa Munisi, fedha hizo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, yakiwamo afya, elimu na mafunzo ya ufundi kwa jamii zinazozunguka mgodi.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu, Rhys Harvey, alieleza hatua zinazotekelezwa na mgodi katika kuimarisha usalama wa wafanyakazi, ikiwamo matumizi ya teknolojia katika shughuli za uchimbaji.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, alishiriki katika ziara hiyo iliyolenga kutathmini utekelezaji wa kanuni za usalama na afya mahali pa kazi katika shughuli za mgodi.

Katika ziara hiyo, Mbunge wa Temeke, Mariam Kisangi, alitaka watu wenye ulemavu wapewe kipaumbele zaidi katika fursa za ajira na miradi ya uwajibikaji kwa jamii inayotekelezwa na mgodi.

Kisangi alisema ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika fursa hizo unaweza kuwawezesha kupata kipato na kushiriki katika shughuli za maendeleo zinazotokana na uwepo wa mgodi katika eneo hilo.

Akijibu hoja hiyo, Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Bulyanhulu, Agapith Paul, alisema mgodi umejenga Shule ya Msingi Segese kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu na kuweka mazingira pamoja na vifaa vinavyowawezesha kupata elimu.

Ziara hiyo imeangazia athari za shughuli za uchimbaji kwa usalama na afya ya wafanyakazi, utekelezaji wa sheria za kazi, matumizi ya teknolojia katika kuongeza usalama, pamoja na mchango wa mgodi katika maendeleo ya jamii zinazouzunguka.

Posted in

Leave a comment