
Na George Gabriel
Wananchi wa Masuguru, Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, wameanza kunufaika na huduma ya maji baada ya kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma–Mangaka, ambao umewaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Wananchi hao wamesema upatikanaji wa huduma hiyo umewapa unafuu mkubwa katika maisha yao ya kila siku, hasa kutokana na kupungua kwa adha ya kubeba ndoo za maji kichwani na kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua mradi huo katika eneo la Masuguru jana, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliwapongeza viongozi, wataalamu na mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya M/S AFCONS Infrastructure, kwa kufanikisha kukamilika kwake.

Mradi huo tayari umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu yake ili huduma hiyo iwe endelevu.
Waziri Aweso aliwaelekeza wananchi na viongozi kuhakikisha miundombinu ya mradi inatunzwa na huduma inatolewa kwa ufanisi, ili wananchi wanufaike kikamilifu na uwekezaji uliofanywa na Serikali.
Aidha, Waziri Aweso alitoa maelekezo ya kuhakikisha huduma ya maji kutoka katika mradi huo inapanuliwa hadi eneo la Mtambaswala, kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, Mhe. Yahya Ally Mhata.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wananchi wa Mtambaswala kupata huduma ya maji kupitia mradi huo.
Akizungumza na wananchi, Aweso alisema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu.
Kufuatia kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa mradi huo, Waziri Aweso alimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu kiasi cha Shilingi milioni tano kwa ajili ya wananchi wa Masuguru kusherehekea hatua hiyo ya upatikanaji wa huduma ya maji.

Kwa upande wao, wananchi Mjarufu Adam na Mariam Issa waliishukuru Serikali kwa kukamilisha mradi huo, wakisema huduma ya maji imewaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu na kubeba ndoo kichwani wakitafuta maji.
Walisema huduma hiyo imeleta unafuu mkubwa katika maisha yao ya kila siku na wanaamini mradi huo utaendelea kuboresha maisha ya wananchi na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Mradi wa Mto Ruvuma–Mangaka ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Leave a comment