Na Andrea Mlwafu

UBALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania umeitaka Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuongeza kasi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), huku mwaka 2030 ukiendelea kukaribia.

Wito huo umetolewa jana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoets, wakati wa hafla ya kupandisha bendera ya Malengo ya Maendeleo Endelevu iliyofanyika katika Makao Makuu ya Kanda ya Umoja wa Ulaya (EU), Dar es Salaam.

Crompvoets alisema nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilijitolea kutekeleza Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030 kwa lengo la kujenga dunia yenye ustawi, amani na usalama kwa wote, huku likisisitizwa suala la kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.

Alisema Malengo ya Maendeleo Endelevu ni miongoni mwa nyenzo muhimu za kufikia malengo yaliyowekwa katika Ajenda ya 2030, ingawa changamoto zilizopo zinaweza kufanya iwe vigumu kwa baadhi ya malengo kufikiwa kikamilifu kabla ya mwaka huo.

“Tunajua mwaka 2030 unakaribia na itakuwa changamoto kufikia Malengo yote ya Maendeleo Endelevu. Hata hivyo, ni muhimu kuendelea kuyakumbuka na kuweka mkazo katika malengo hayo kila mwaka,” alisema Crompvoets.

Alisema elimu bora ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele zaidi, akitaja pia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa eneo linalohitaji juhudi zaidi.

Kwa mujibu wa Crompvoets, wakati baadhi ya nchi zikiendelea kukabiliana na changamoto za umaskini na njaa, Tanzania imeanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema Uholanzi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yanayohusiana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, yakiwemo maendeleo ya viwanda, ubunifu na miundombinu.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Chikulupi Kasaka, alisema hafla hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka Tanzania na nje ya nchi kwa ajili ya kukumbushana kuhusu utekelezaji wa ahadi na malengo yaliyowekwa katika Ajenda ya Maendeleo Endelevu.

Kasaka alisema Ubalozi wa Uholanzi umekuwa ukiongoza katika kuadhimisha siku hiyo kila Septemba kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzikumbusha nchi kuhusu ahadi walizojiwekea katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Alisema hafla hiyo pia inatoa fursa kwa nchi kutathmini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa malengo hayo, kubaini maeneo yaliyopiga hatua na yale ambayo bado yanahitaji juhudi zaidi.

“Tukio hili linatoa nafasi ya kukumbusha nchi kwamba Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030 inakaribia mwisho na muda uliobaki wa kufikia malengo hayo ni mchache,” alisema Kasaka.

Hafla hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kila mwaka ya kuhamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, huku mwaka 2030 ukiendelea kusogea kama mwisho wa kipindi kilichowekwa na Umoja wa Mataifa kwa utekelezaji wa malengo hayo.

Malengo ya Maendeleo Endelevu yanahusisha maeneo mbalimbali ya maisha ya wananchi, yakiwemo kupunguza umaskini na njaa, kuboresha elimu na afya, kulinda mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kukuza ajira na uchumi jumuishi pamoja na kujenga taasisi zenye ufanisi.

Kwa Tanzania, utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu unaendelea kuhusishwa na mipango ya kitaifa ya maendeleo, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iliyoanza kutekelezwa rasmi Julai 1, 2026.

Posted in

Leave a comment