
Na Andrea Mbona, Mbulu
Matumizi ya pombe miongoni mwa waendesha bodaboda yameelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia ajali za barabarani, huku madereva wakitakiwa kuepuka ulevi hasa wanapokuwa kazini.
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Mbulu, Cpl Octavian, ametoa rai hiyo wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda katika eneo la stendi ya bodaboda Mbulu.
Alisema pombe huwafanya baadhi ya madereva kujiamini kupita kiasi na kupunguza umakini wakati wa kuendesha, hali inayoweza kusababisha uzembe na ajali zinazosababisha vifo, majeraha na ulemavu.
“Acheni kunywa pombe na kuendesha pikipiki. Ni hatari sana na ni sababu kubwa ya ajali nyingi,” alisema Cpl Octavian.
Aidha, aliwataka waendesha bodaboda kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani wakati wote wanapokuwa kazini ili kujilinda wao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodaboda wa kijiwe cha stendi, Amani Daniel, amemshukuru askari huyo kwa elimu hiyo, akisema ulevi umekuwa ukihusishwa na baadhi ya ajali zinazowahusisha waendesha pikipiki.

“Ni kweli afande, kuhusu ulevi mara nyingi ajali zinapotokea tumekuwa tukiwakuta madereva wengi wakiwa katika hali ya ulevi, hivyo tunashukuru kwa kutukumbusha,” alisema Amani.
Leave a comment