Na Pilastus Nyaulingo

Wanaishi nyumba moja. Wanalala kitanda kimoja. Wanaweza hata kula chakula mezani pamoja. Lakini wakati mwingine au wakati wote, kila mmoja anaishi katika dunia yake.

Mmoja anashika simu kuangalia WhatsApp. Mwingine anaingia Instagram, TikTok au Facebook. Dakika zinapita, saa zinapita, siku zinapita mazungumzo yanapungua na ukimya unatawala.

Kwa nje, ndoa inaonekana na kila kitu kinachohitajika. Lakini ndani yake, mmoja au wote wawili wanaweza kuwa wanapitia hisia za upweke.

Hapo ndipo simu inapoanza kupata nafasi nyingine katika maisha ya wanandoa. Badala ya kuwa chombo cha kuwasiliana tu, simu inaweza kuwa sehemu ya kukimbilia wakati mtu anahisi hana mtu wa kuzungumza naye. Inaweza kumpa burudani, mazungumzo na watu wengine au hisia ya kwamba kuna mtu anayemsikiliza.

Lakini swali linabaki: Je, simu inawasaidia wanandoa kukabiliana na upweke, au wakati mwingine inazidi kuwapeleka mbali zaidi?

UPWEKE UPO HATA KATIKA NDOA

Tunaposema mtu yuko peke yake, mara nyingi tunafikiria mtu asiye na mwenza, familia au marafiki. Lakini upweke unaweza kuwa tofauti. Mtu anaweza kuwa na mwenza lakini akahisi hana mtu anayemsikiliza, anayemwelewa au anayeshirikiana naye kihisia.

Katika ndoa, hususani za miongo hii, hali hii hujitokeza mawasiliano yanapopungua, wanandoa wanapokuwa na ratiba zinazowatenganisha, migogoro inapokaa muda mrefu bila kutatuliwa au kila mmoja anapojenga maisha yake bila kumshirikisha mwenzake.

Utafiti wa Mhadhiri Msaidizi katika Idara ya Uandishi wa Habari na Masomo ya Mawasiliano, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Vincent Mpepo wa mwaka 2017, uliohusu athari za mitandao ya kijamii katika mawasiliano ya wanandoa katika Mkoa wa Dar es Salaam, ulihusisha washiriki 117 kutoka Ilala, Kinondoni na Temeke.

Utafiti huo ulionyesha kuwa mitandao ya kijamii inaweza kuwa na mchango chanya katika mawasiliano ya wanandoa. Asilimia 80 ya washiriki walisema mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii yalisaidia kuimarisha uhusiano wao, huku asilimia 12 wakiwa hawana uhakika na asilimia nane wakisema hayakusaidia kuimarisha uhusiano.

Mpepo alipendekeza wanandoa kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuwa makini na masuala ya faragha na usiri katika matumizi ya teknolojia hiyo.

Hapa ndipo tunapoona kwamba tatizo si simu yenyewe. Tatizo linaweza kuwa namna simu na mitandao ya kijamii vinavyotumiwa ndani ya mahusiano.

SIMU INAPOKUWA MAHALI PA KUKIMBILIA

Kwa mwanandoa anayehisi kupuuzwa au kutosikilizwa, simu inaweza kuwa na mvuto mkubwa.

Anaweza kuingia kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kuzungumza na watu wengine. Anaweza kutazama video kwa muda mrefu, kusoma maoni, kushiriki kwenye vikundi au kuwasiliana na rafiki ambaye anahisi anamwelewa zaidi.

Hapo simu inaweza kuanza kufanya kazi kama aina ya rafiki wa kidijitali.

Tatizo linatokea ambapo muda unaotumika kutafuta faraja kwenye simu unaanza kuchukua nafasi ya muda ambao ungeweza kutumika kujenga, kuboresha uhusiano wa wanandoa.

Katika utafiti huo wa mwaka 2017 unaonyesha upande mmoja muhimu wa jambo hili: mitandao ya kijamii inaweza kusaidia wanandoa kuwasiliana na kuimarisha uhusiano wao, lakini matumizi yake yanahitaji mipaka na uelewa wa namna yanavyoweza kuathiri faragha na mawasiliano ya wanandoa.

Kwa hiyo, simu inaweza kuwa daraja la mawasiliano au ikawa njia ya kukwepa mazungumzo ya ana kwa ana, kutegemea namna inavyotumiwa.

WANANDOA WANAWEZA KUWA KARIBU KIDIJITALI LAKINI MBALI KIHISIA

Mwanandoa anaweza kutuma ujumbe kwa mwenza wake akiwa kazini. Anaweza kumpigia simu, kumtumia picha au hata kumjibu ndani ya sekunde chache au pia asijibu huku pia mwenza anaweza kuona aina fulani ya kupuuzwa.

Lakini mawasiliano yote hayo yanaweza kuwepo huku mazungumzo muhimu ya ndani ya ndoa yakikosekana.

“Unaendeleaje?” inaweza kuulizwa, lakini hakuna anayefika kwenye swali la “Umeshindaje?”

Hapo ndipo tofauti kati ya mawasiliano na ukaribu wa kihisia vinapoonekana.

Utafiti wa Estella Alfred Mwambene wa mwaka 2019 kuhusu matumizi ya simu katika ndoa huko Iringa uliangalia namna matumizi ya teknolojia yanavyoathiri maisha ya familia na mawasiliano ya wanandoa.

Utafiti huo ulihusisha wanandoa pamoja na viongozi wa jamii na watoto, na uliangazia namna simu zinavyoweza kusaidia mawasiliano lakini pia kuleta changamoto pale matumizi yanapokuwa ya kupita kiasi.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa uwezo wa kuwasiliana kwa simu siyo lazima kubebe maana halisi ya ukaribu wa kihisia kwa wanandoa hao.

Mwanandoa anaweza kuwa anawasiliana kila siku na mwenza wake kupitia simu, lakini bado akahisi hasikilizwi, haeleweki au anapuuzwa.

SIMU INAPOCHUKUA NAFASI YA MWENZA….

Kuna wakati mtu haishiki simu kwa sababu ana jambo maalumu la kufanya. Anaishika kwa sababu amezoea.

Anaangalia ujumbe. Anafungua TikTok. Anarudi WhatsApp. Anaangalia Instagram na katika mitandao mingine au programu tumizi.

Kwa mwanandoa anayehisi upweke, mzunguko huu unaweza kumpa hisia ya kuwa ana watu karibu naye.

Lakini ukaribu wa kidijitali si lazima uwe sawa na ukaribu wa kihisia.

Mtu anaweza kupata jumbe nyingi mtandaoni lakini bado akahisi hana mtu wa kumweleza kinachomsibu moyoni.

Hili linafanya swali la matumizi ya simu ndani ya ndoa kuwa kubwa kuliko suala la muda wa kutumia skrini. Linakuwa suala la mahusiano.

SIMU NA MIGOGORO YA NDOA…

Mwaka 2026, Haji Ally Mkande kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii ya Jamii Tengeru alichapisha utafiti uliochunguza matumizi na athari za simu katika migogoro ya ndoa mkoani Dar es Salaam.

Utafiti huo ulihusisha washiriki 30, wakiwemo wanaume 10 waliooa, wanawake 10 walioolewa, wakwe wanne, watoto wanne na maafisa wawili wa ustawi wa jamii.

Utafiti huo ulionyesha kuwa simu zinaweza kuwa chombo muhimu cha mawasiliano kati ya wanandoa, lakini matumizi yasiyofaa yanaweza pia kuongeza migogoro, hasa pale yanapohusisha usiri, mawasiliano ya nje ya ndoa na tuhuma za kutokuwa waaminifu.

Hii inaonyesha kuwa simu si lazima iwe chanzo pekee cha migogoro ya ndoa. Wakati mwingine inaweza kuwa chombo kinachorahisisha au kuonyesha matatizo ambayo tayari yapo ndani ya uhusiano.

USIRI WA SIMU UNAPOJENGA UKUTA…

Kuna tofauti kati ya kuwa na faragha na kuwa na usiri.

Kila mwanandoa ana haki ya kuwa na nafasi yake binafsi. Lakini pale simu inapokuwa eneo ambalo mwenza haruhusiwi kabisa kulikaribia, kila ujumbe unafichwa, kufutwa na matumizi yake yanaambatana na hofu ya kugundulika, mashaka yanaweza kuanza.

Mwanandoa anaweza kujiuliza: “Kwa nini simu yake siku zote iko kimya?” “Kwa nini akipokea simu anatoka nje?” “Kwa nini ujumbe fulani unafutwa?” “Kwa nini muda mwingi anaonekana kuwa karibu na watu wa mtandaoni kuliko mimi?”

Maswali haya yanaweza kuzaa mashaka hata kabla ya mtu kuwa na ushahidi wa jambo lolote.

Utafiti wa Mkande unaonyesha umuhimu wa kuangalia namna matumizi ya simu yanavyohusiana na migogoro ya ndoa, mawasiliano na masuala ya uaminifu.

Kwa hiyo, tatizo linaweza lisianze na usaliti wenyewe, bali linaweza kuanza na kuvunjika kwa uaminifu na mawasiliano.

SIMU INAWEZA PIA KUWA SEHEMU YA SULUHISHO

Pamoja na changamoto hizo, si sahihi kuifanya simu ionekane kama adui wa ndoa.

Kwa wanandoa wanaoishi mbali kutokana na kazi, biashara au majukumu mengine, simu inaweza kuwa muhimu sana.

Mwanandoa anaweza kumpigia mwenza wake wakati wa mapumziko kazini, kumjulisha anachofanya, kumjulia hali au kumtumia ujumbe wa kumtia moyo.

Mitandao ya kijamii pia inaweza kuwa sehemu ya kushirikishana mambo yanayowafurahisha.

Utafiti wa Mpepo wa mwaka 2017 unaunga mkono upande huu chanya. Asilimia 80 ya washiriki wake walisema mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii yalisaidia kuimarisha uhusiano wao.

Kwa hiyo, suala si kuondoa simu kwenye ndoa. Ni kuhakikisha simu haiondoi ndoa kwenye maisha ya wanandoa.

WAKATI SIMU INAPOCHUKUA NAFASI YA MAZUNGUMZO

Fikiria wanandoa wawili wamekaa sebuleni.

Mume anaangalia simu. Mke anaangalia simu.

Wote wako pamoja, lakini hakuna anayezungumza na mwenzake.

Hii inaweza kuonekana kama jambo dogo, lakini ikiwa ni tabia ya kila siku na endelevu, inapunguza muda wa mawasiliano ya ana kwa ana.

Utafiti wa mwaka 2019 kuhusu matumizi ya simu mahiri katika ndoa huko Iringa ulionyesha changamoto zinazoweza kujitokeza pale simu zinapotumika kupita kiasi, ikiwemo kuvurugika kwa mawasiliano ya ana kwa ana na muda wa familia.

Hapo ndipo matumizi ya simu yanapohitaji mipaka.

Siyo kila dakika ya mapumziko lazima ijazwe na matumizi ya simu au skrini.

Wakati mwingine ndoa inahitaji dakika chache ambazo hakuna anayeshika simu.

UPWEKE HAUJIBIWI KWA DATA,BANDO PEKEE

Kuna jambo moja muhimu ambalo wanandoa wanapaswa kulifikiria.

Kama mtu anatumia simu kila usiku kwa sababu hataki kukaa kimya na mwenza wake, huenda tatizo si simu.

Huenda kuna mazungumzo ambayo hayajafanyika.

Huenda kuna maumivu ambayo hayajasikilizwa.

Huenda kuna migogoro ambayo imeachwa kwa muda mrefu.

Huenda mmoja anahisi hapendwi, au anapuuzwa.

Au huenda wote wawili wamekuwa wakiishi ndani ya ratiba yenye majukumu mengi kiasi kwamba wamesahau kujenga urafiki wao wenyewe.

Katika hali kama hiyo, simu inaweza kutoa usumbufu wa muda lakini isitatue chanzo cha upweke.

Ni dhahiri mazungumzo yanahitajika kati ya wanandoa ili kubaini chanzo cha upweke huo na kupatikana kwa suluhu isiyohusisha matumizi ya simu kama kimbilio au kichaka cha upweke.

WANANDOA WANAHITAJI KUJENGA MUDA WAO

Kuna umuhimu wa wanandoa kuwa na muda ambao ni wao.

Muda wa kuzungumza, muda wa kula pamoja, muda wa kutembea. Muda wa kucheka, muda wa kuzungumzia fedha, watoto, kazi, mahusiano yao na mambo yanayowasumbua.

Na wakati mwingine, muda wa kukaa bila simu.

Hili si suala la teknolojia pekee. Ni suala la kuweka uhusiano mbele wakati ambapo kila mmoja anaweza kuwa na ulimwengu wake wa kidijitali.

Utafiti wa mwaka 2024 kuhusu mahusiano ya wanandoa na mitandao ya kijamii ulionyesha kuwa matumizi ya mitandao yanaweza kuathiri namna wanandoa wanavyowasiliana na kuhusiana, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuweka mipaka na kuwa na mawasiliano ya wazi kuhusu matumizi ya teknolojia ndani ya ndoa.

SIMU ISIWE SEHEMU YA KUFICHA UPWEKE

Mwanandoa anayejihisi mpweke si lazima aihitaji simu zaidi ya mwenza wake.

Anaweza kuwa anahitaji mwenza wake zaidi.

Anahitaji kuzungumza.

Anahitaji kusikilizwa.

Anahitaji kuulizwa anaendeleaje bila mazungumzo kuishia kwenye bili, watoto, chakula, kazi au majukumu ya nyumbani.

Kwa sababu ndoa inaweza kuwa na kila kitu kinachoonekana nje lakini ikawa na upweke mkubwa ndani.

Na wakati huo, simu inaweza kuwa rahisi zaidi kuishika kuliko kumtazama mwenza machoni na kusema:

“Nahisi niko peke yangu.”

Hilo ndilo jambo ambalo wanandoa wanahitaji kulifikiria.

TEKNOLOJIA ISIJENGE UKUTA KATI YA WENZA

Simu imebadilisha namna tunavyowasiliana. Imefanya iwe rahisi kumpata mwenza aliye mbali, kutuma ujumbe, kupiga video na kushirikishana maisha ya kila siku.

Lakini teknolojia hiyo hiyo inaweza kuwa chanzo cha umbali ikiwa itaanza kuchukua nafasi ya mawasiliano ya kweli.

Tafiti za Tanzania za mwaka 2017, 2019 na 2026 zinaonyesha namna tofauti kwamba simu na mitandao ya kijamii zinaweza kuwa na faida katika mahusiano, lakini matumizi yasiyo na mipaka yanaweza pia kuvuruga mawasiliano, kuongeza usiri, kuathiri uaminifu na kuleta migogoro.

Kwa hiyo, suluhisho si kuwaambia wanandoa waache kutumia simu.

Suluhisho ni kujenga utamaduni ambao simu inakuwa chombo cha kuimarisha ndoa, si mahali pa kukimbilia kila mmoja anapohisi mpweke.

Kwa sababu mwisho wa siku, mtu anaweza kuwa na maelfu ya watu kwenye simu yake lakini bado akahitaji mtu mmoja tu aliyeko pembeni yake, na si mwingine ni mwenza wake.

Na kama mtu huyo ni mwenza wake, basi labda kabla hajafungua simu kutafuta mtu wa kuzungumza naye, anapaswa kwanza kuuliza:

“Tumepata lini muda wa kuzungumza?”

Huenda jibu la upweke ndani ya ndoa lisianzie kwenye simu. Huenda linaanzia kwenye mazungumzo yaliyokosekana kati ya watu wawili wanaoishi chini ya paa moja.

Posted in

Leave a comment