Na Furahisha Nundu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Jumapili, Oktoba 4, 2026, amesimikwa rasmi kuwa Kanoni Mlei wa Kanisa Anglikana Tanzania katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana la Kristo Mfalme, Chanika, Dayosisi ya Handeni, mkoani Tanga.

Tukio hilo limefanyika katika ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu kwa Kasisi Canon Charles Mika Lundu kuwa Askofu wa Dayosisi ya Handeni, ambapo Dkt. Mwigulu alishiriki ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Mwigulu alitunukiwa cheo cha Kanoni Mlei na Kanisa Anglikana Tanzania chini ya uongozi wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Maimbo Mndolwa, Juni 21, 2026, katika harambee ya kukamilisha mradi wa jengo la Kitega Uchumi cha Kanisa Anglikana Tanzania iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo la Dodoma.

Kanisa Anglikana Tanzania lilimtunuku Waziri Mkuu cheo hicho kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha na kufanikisha uchangishaji wa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na vitega uchumi vya Kanisa hilo, tangu alipokuwa akitumikia nyadhifa mbalimbali serikalini na katika jamii.

Kutunukiwa cheo hicho na kusimikwa rasmi leo katika ibada iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dkt. Maimbo Mndolwa, kumemfanya Waziri Mkuu kuungana na viongozi wengine wa Serikali waliowahi kutunukiwa wadhifa huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dkt. Nchemba ni wa kwanza kutoka nje ya dhehebu la Anglikana kutunukiwa wadhifa wa Kanoni Mlei wa Kanisa hilo.

Viongozi wengine waliowahi kutunukiwa cheo cha Kanoni Mlei (Lay Canon) ni pamoja na Spika Mstaafu, Hayati Job Yustino Ndugai; Jaji Mkuu Mstaafu, Hayati Augustino Steven Lawrence Ramadhani; na Profesa Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu).

Wengine ni Baraka Leonard, Katibu wa Bunge, pamoja na Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo.

Kwa mujibu wa taratibu za Kanisa Anglikana, Kanoni Mlei ni cheo cha heshima katika Kanisa hilo, ambacho miongoni mwa majukumu yake ni kutoa ushauri na kuwa mlezi wa uongozi wa juu wa Kanisa.

Posted in

Leave a comment