Na Mwandishi Wetu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewakamata Razaki Makolo na Luka Dotto, wakazi wa Mabatini, Wilaya ya Chunya, kwa tuhuma za kumuua Sira John (20) kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, tukio hilo lilitokea Septemba 30, 2026, katika Kitongoji cha Mabatini, Kata ya Chokaa, baada ya marehemu na watuhumiwa kudaiwa kunywa pombe pamoja na kisha kutokea ugomvi.

Inadaiwa kuwa baada ya kuondoka katika kilabu hicho, Sira alikutana na watuhumiwa akiwa njiani kuelekea kambini alipokuwa akifanyia kazi. Watuhumiwa hao wanadaiwa kumvizia na kumchoma sehemu mbalimbali za mwili, hali iliyosababisha kifo chake.

Kamanda Kuzaga amesema Polisi, kupitia Kikosi Maalum cha Kupambana na Mauaji, ilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Katika misako na operesheni zilizofanyika mwezi Septemba, Polisi pia iliwakamata watuhumiwa 29 waliokuwa na jumla ya kilo 13.816 za bangi, watuhumiwa wanane waliokuwa na lita 90 za gongo, watuhumiwa 15 waliokuwa na bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh milioni 3.3, pamoja na mtuhumiwa mmoja aliyekuwa na silaha aina ya gobore bila kibali.

Posted in

Leave a comment