Na Abel Mwakingwe

Serikali imewataka wadau wanaosimamia programu ya mikopo kwa kampuni changa za TEHAMA kuhakikisha Sh bilioni tano zilizotengwa kuwawezesha vijana zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayoweza kupimika.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ametoa wito huo hivi karibuni jijini Dodoma wakati akizindua programu inayolenga kuongeza uwezo wa kampuni changa kupata mitaji kwa ajili ya kukuza biashara na ubunifu.

Kairuki alisema utekelezaji wa programu hiyo unapaswa kuangalia zaidi matokeo yatakayopatikana kwa wanufaika, ikiwemo ukuaji wa kampuni, uundaji wa ajira, ongezeko la mauzo na mapato, upanuzi wa masoko pamoja na urejeshaji wa mikopo.

Alisema mikopo hiyo itatolewa kwa makundi matatu kulingana na mahitaji ya biashara. Kiwango cha kwanza ni kuanzia Sh milioni moja hadi Sh milioni 25, cha pili ni zaidi ya Sh milioni 25 hadi Sh milioni 100, na kiwango cha juu ni zaidi ya Sh milioni 100 hadi Sh milioni 500.

Katika hatua nyingine, Kairuki aliitaka Tume ya TEHAMA kukamilisha mwongozo utakaowezesha kampuni changa za TEHAMA kushiriki katika zabuni za Serikali na kuuwasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa hatua zinazofuata.

Aidha, aliziagiza Wizara, Tume ya TEHAMA na Benki ya Azania kuweka mfumo maalumu wa kufuatilia matokeo ya programu hiyo, ikiwemo maendeleo ya kampuni zitakazonufaika na namna zitakavyotumia fedha hizo.

Kwa upande wa kampuni zinazolengwa, Waziri huyo amewataka wabunifu kujisajili kupitia Mfumo wa Jamii Hunt, ambao umetajwa kuwa njia rasmi ya utambuzi na uwasilishaji wa maombi ya programu hiyo.

Pia, amewataka wabunifu kuangalia uwezekano wa kuunda umoja rasmi kwa kuzingatia sheria na taratibu, akisema hatua hiyo inaweza kurahisisha uwakilishi wao na kusaidia kutambua changamoto pamoja na mahitaji yao.

Kairuki alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mpango wa kutoa elimu kwa umma ili kampuni changa na wabunifu waelewe vigezo vya kupata mikopo, namna ya kuomba, wajibu wa wanufaika na manufaa yanayotarajiwa kutokana na programu hiyo.

Alisema wanufaika wanapaswa kutumia fedha hizo kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kukuza biashara zao na kutafuta masoko ya ndani na nje ya Tanzania ili kuongeza mchango wa kampuni changa katika sekta ya TEHAMA.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya, alisema benki hiyo itashirikiana na Wizara katika kufanya tathmini na kutoa mikopo kwa kampuni zitakazokidhi vigezo vilivyowekwa.

Alisema pamoja na fedha, kampuni zitakazonufaika zitapatiwa pia ujuzi kuhusu usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu na uandaaji wa mipango ya biashara, hatua inayolenga kusaidia kujenga kampuni zenye uwezo wa kukua, kuendelea na kuzalisha ajira.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waanzilishi wa Biashara Bunifu Tanzania (TSA), Zahoro Muhaji, ambaye pia alizungumza kwa niaba ya chama hicho upande wa Zanzibar, aliwataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha inarejeshwa ili kuwawezesha wabunifu wengine kunufaika.

Alisema matumizi yenye tija na urejeshaji wa mikopo ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kujenga uaminifu na kuwezesha fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya TEHAMA.

Posted in

Leave a comment