
Na Pilastus Nyaulingo
WAKAZI wa Dar es Salaam wanaotupa taka ovyo, kumwaga uchafu kwenye mifereji, mito na maeneo ya wazi wanakabiliwa na faini ya hadi Sh milioni moja, huku mamlaka za jiji zikianza kuimarisha utekelezaji wa sheria za usafi na usimamizi wa mazingira.
Hatua hiyo inatekelezwa chini ya Sheria Ndogo za Usafi na Usimamizi wa Mazingira za Jiji la Dar es Salaam za mwaka 2024, ambazo mamlaka zimesema zitatekelezwa kikamilifu katika maeneo yote ya jiji.
Akizungumza kuhusu utekelezaji huo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alisema makosa yatakayochukuliwa hatua ni pamoja na kutupa taka barabarani, kumwaga uchafu kwenye mifereji, mito na maeneo ya wazi, kujisaidia katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuosha magari katika maeneo yasiyotengwa.
“Kitendo cha mtu kutupa karatasi ya pipi au ganda la ndizi barabarani kinaweza kuchukuliwa kuwa kosa chini ya sheria hizo,” alisema Mpogolo.
Mpogolo alisema utekelezaji utaanza kwa kutumia kiwango cha juu cha faini kilichowekwa katika sheria, huku akiwataka wakazi kuzingatia wajibu wao wa kutunza mazingira.
Alisema vijana wataajiriwa kuwa wakaguzi na kupewa pikipiki zitakazowawezesha kufuatilia utekelezaji wa sheria katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alisema utekelezaji wa sheria hizo utahusisha kata zote 36 za jiji.

Mabelya alisema halmashauri itashirikiana na wananchi, viongozi wa maeneo, wafanyabiashara na wadau wa mazingira kutoa elimu kuhusu wajibu wa kila mmoja katika kutunza mazingira.
Aidha, mamlaka zimepanga kuongeza mapipa ya taka katika maeneo mbalimbali ya jiji na kuendesha kampeni za elimu kwa wananchi kuhusu sheria na adhabu zinazohusiana na uchafuzi wa mazingira.
Katika hatua nyingine, waendeshaji wa usafiri wa umma, wakiwemo daladala na bajaji, watahusishwa katika ukaguzi wa mazingira katika maeneo ya usafiri kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na maafisa wa afya.
Utekelezaji huo unafanyika baada ya Serikali kutoa maelekezo ya kuimarisha usafi katika miji na manispaa, sambamba na kuandaa mipango ya muda mrefu ya usimamizi wa taka.
Mamlaka zimewataka wakazi wa Dar es Salaam kutambua kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la pamoja na kwamba kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kulinda afya ya jamii na mazingira.

Leave a comment