
Na Grace Mwakalinga
Wadau wa sekta ya utalii nchini wametakiwa kuongeza matumizi ya Akili Unde (AI) na teknolojia za kisasa katika kutangaza vivutio, kuboresha huduma na kurahisisha upatikanaji wa taarifa pamoja na upangaji wa safari kwa watalii.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani na uzinduzi wa mfumo wa eSIM Card unaolenga kuwaunganisha watalii na watoa huduma za utalii.
Chande amesema maendeleo ya teknolojia yamebadili namna watalii wanavyotafuta taarifa, kuchagua maeneo ya kutembelea, kupanga safari, kuweka nafasi na kushirikisha uzoefu wao, hivyo Tanzania inapaswa kwenda sambamba na mabadiliko hayo.
“Kaulimbiu ya mwaka huu inatukumbusha kuwa utalii wa sasa hauwezi kutenganishwa na teknolojia. Watalii wanatumia teknolojia kutafuta taarifa, kuchagua maeneo ya kutembelea, kupanga safari, kufanya booking na kushirikisha uzoefu wao,” alisema Chande.
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta hiyo, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha teknolojia inazalisha matokeo katika kuongeza idadi ya watalii, kuboresha huduma na kuongeza thamani ya utalii kwa Taifa.
Chande alisema matumizi ya Akili Unde yanaweza kusaidia sekta ya utalii kukidhi mahitaji ya mtalii wa kisasa, ambaye anazidi kutumia majukwaa ya kidijitali kupata taarifa na kufanya maamuzi kuhusu safari.
Alisema mfumo wa eSIM Card unalenga kumrahisishia mtalii kupata taarifa muhimu wakati wa maandalizi na utekelezaji wa safari, ikiwemo taarifa kuhusu vivutio, huduma za malazi, usafiri na huduma nyingine za utalii.
Alisema mfumo huo ni sehemu ya ubunifu unaolenga kuunganisha teknolojia na uuzaji wa Tanzania kama eneo la utalii.
Amepongeza jitihada zinazofanywa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) za kuendelea kuunganisha teknolojia na uuzaji wa maeneo ya utalii nchini, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uwezo wa Taifa wa kumfikia mtalii moja kwa moja na kumpatia taarifa na huduma kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa TTB, Paulina Mkama, aliwataka wananchi kushiriki katika kukuza utalii wa ndani kwa kutumia teknolojia, hususan simu janja, kutafuta taarifa sahihi na kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Paulina amesema Tanzania ina fursa nyingi za utalii ambazo hazipaswi kuishia katika hifadhi za wanyamapori pekee, bali zinahusisha pia historia, utamaduni, vyakula, fukwe, milima na maeneo ya urithi yaliyopo katika sehemu mbalimbali za nchi.
Alisema wananchi wanapaswa kuanza kwa kuvifahamu vivutio vilivyopo nchini, kuvitembelea na kushirikisha wengine uzoefu wao, hatua ambayo inaweza kusaidia kuongeza uelewa na hamasa ya utalii wa ndani.

“Wananchi wanaweza kutumia simu zao janja kutafuta taarifa kuhusu vivutio vilivyopo katika maeneo mbalimbali, namna ya kuvifikia na huduma zinazopatikana,” alisema Mkama.
Mkama alisema wataalamu wa utalii waliopo katika maeneo mbalimbali nchini wanaweza pia kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu vivutio, historia ya maeneo hayo na huduma zinazopatikana.
Alisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na upatikanaji wa taarifa sahihi ili wananchi na watalii waweze kufanya maamuzi sahihi wanapopanga safari.
Kaulimbiu ya Siku ya Utalii Duniani mwaka huu ni “Ajenda ya Kidijitali na Akili Unde katika Kubuni Upya Utalii,” ikisisitiza nafasi ya teknolojia na Akili Unde katika mabadiliko ya sekta hiyo.

Leave a comment