
Na Grace Mwakalinga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hai kimepanga kuitisha kikao cha Kamati ya Siasa kujadili sakata la Mwenyekiti wa CCM Kata ya Bomang’ombe, Agness Kimaro, aliyedai kuwekwa ndani kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko.
Kimaro alikamatwa Septemba 25, 2026, wakati akielekea kwenye shughuli za ujenzi wa shina la CCM, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hai, Wang’uba Maganda, alisema chama hicho kimepata taarifa kuhusu tukio hilo, lakini suala hilo halijawasilishwa rasmi katika ofisi ya chama.
Alisema kutokana na sakata hilo kupata mwangwi mkubwa, wameamua kuitisha kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ili kulijadili kwa kina, kubaini chanzo cha tukio, namna lilivyotokea na hatua zilizochukuliwa.
“Kwa sababu halijafika mezani kwetu rasmi, hatukuliingilia kwa namna yoyote katika mchakato huo, lakini kwa sasa, kwa sababu limepata mwangwi mkubwa nchini, tumekubaliana tufanye kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ili kulijadili,” alisema Maganda.
Alisema baada ya kikao hicho, chama kitatoa msimamo kuhusu suala hilo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Kimaro alisema baada ya kuachiliwa alielezwa na polisi kuwa walikuwa wameagizwa kumpeleka kituoni, kabla ya kuambiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ndiye aliyeagiza apelekwe kwake.
Hata hivyo, Bomboko alikanusha kuhusika na kukamatwa kwa Kimaro, akisema hana taarifa kuhusu tukio hilo.
“Sina hizo taarifa mimi. Mimi nasikia kwako. Ikiwa zipo kwenye mitandao ya kijamii, naomba nikutumie namba yangu ya WhatsApp unitumie hiyo taarifa ili niweze kuiona kabla ya kuongea. Maana si kweli, mimi sijamkamata mtu na sina hiyo taarifa,” alisema Bomboko.
Kimaro aliachiwa kwa dhamana iliyowekwa na Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe, na kurejeshwa katika ofisi za chama.
Leave a comment