Na Grace Mwakalinga
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametakiwa kuchukua hatua za haraka kumaliza mgogoro wa madereva wa mabasi na malori, huku akitakiwa kuitisha mazungumzo na wadau wa sekta hiyo ili kurejesha huduma za usafiri nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani wa ACT Wazalendo, Naggy Kaboyoka, aliyesema Serikali inapaswa kusitisha kwa muda utekelezaji wa mfumo wa pointi 15 kwenye leseni za madereva na kuzungumza nao kabla ya kuendelea na utekelezaji wake.
Kaboyoka alisema madereva wana hofu kuwa mfumo huo unaweza kusababisha kupoteza pointi kwenye leseni zao na hatimaye kuathiri ajira zao.
Alisema mgogoro huo pia umechangiwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya kanuni za usafirishaji pamoja na kutoshirikishwa kwa madereva na wadau wengine katika maamuzi yanayowahusu.
Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, mgomo huo umeathiri huduma za usafiri na kuwaweka wananchi katika mazingira magumu, wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara, wagonjwa na wasafiri wanaotegemea mabasi na malori.
Wakati huo huo, Katambi amechukua hatua kuhusu mfumo huo kwa kuagiza usitishwe na kueleza kuwa tathmini inapaswa kufanyika, ikiwemo kuzingatia maoni ya wadau.
Katambi pia amewataka madereva kuwa watulivu, huku akisisitiza kuwa hakuna dereva anayepaswa kukatwa pointi kinyume na maelekezo yaliyotolewa.
ACT Wazalendo imesisitiza umuhimu wa Serikali kuhusisha madereva, waajiri na wadau wengine katika mazungumzo ili kupata suluhisho la changamoto zinazolikabili sekta ya usafirishaji na kurejesha huduma za usafiri nchini.
Leave a comment