
Na Iddy Mziray, Songea
Madereva wa mabasi ya abiria mkoani Ruvuma wameendelea na huduma ya usafirishaji baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa huo, SACP Marco Chilya, kuwahakikishia ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kazi.
Chilya alitoa kauli hiyo jana alipokutana na madereva, abiria, wananchi na wadau wa usafirishaji katika Stendi ya Mabasi iliyopo Kata ya Shule ya Tanga, Manispaa ya Songea.
Katika mkutano huo, Kamanda Chilya alisikiliza changamoto zinazowakabili wadau wa usafirishaji na kueleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na idara nyingine linaendelea kuchukua hatua kuhakikisha mazingira ya usafirishaji yanakuwa salama.
Aliwataka madereva kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria na taratibu, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Polisi, madereva, abiria na wadau wengine katika kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea bila vikwazo.

Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa za baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria kusitisha huduma ya usafirishaji kwa sababu mbalimbali, hali iliyokuwa na uwezo wa kuathiri wananchi wanaotegemea usafiri huo katika shughuli zao za kila siku.
Chilya alisema Jeshi la Polisi litaendelea kushughulikia changamoto zinazohusu usalama na kuhakikisha madereva wanafanya kazi katika mazingira salama.
Baada ya mazungumzo hayo, madereva waliendelea na safari zao kama kawaida kuelekea mikoa mbalimbali, hatua iliyowezesha huduma za usafirishaji wa abiria kuendelea na wananchi kuendelea na shughuli zao bila usumbufu wa usafiri.
Mgomo wa madereva wa mabasi na malori ni matokeo ya kupinga mfumo mpya wa kukata pointi kwenye leseni, unaotekelezwa na Kitengo cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi, ambapo dereva anayebainika kufanya makosa barabarani hukatwa pointi 15 kwenye leseni yake.
Mfumo huo umewafanya madereva kusitisha huduma katika stendi mbalimbali nchini wakitaka ufafanuzi na hatua za mfumo huo.

Leave a comment