
Na Cartace Ngajiro – Tanga
Uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga umeongeza shughuli za bandari hiyo na kufungua fursa mbalimbali kwa wananchi, huku ukichangia kukuza mnyororo wa thamani na kuongeza mchango wa bandari katika maendeleo ya Mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Almas Nyangasa, wakati yeye pamoja na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa walipotembelea Bandari ya Tanga kwa lengo la kujifunza na kutazama fursa zinazopatikana katika Mkoa wa Tanga.
Nyangasa alisema uwekezaji huo unaendelea kuleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla, huku akipongeza Serikali kwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza bandari hiyo.
“Tunampongeza Rais wetu kwa dhamira yake ya dhati ya kuwekeza katika Bandari ya Tanga na kuifanya bandari hii kufanya mambo makubwa yenye manufaa kwa taifa,” alisema Nyangasa.
Aidha, aliipongeza Menejimenti ya Bandari ya Tanga kwa usimamizi wa shughuli za bandari, akisema ufanisi huo umechangia kuongezeka kwa shehena na mapato.
Akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya Bandari ya Tanga, Meneja wa Bandari hiyo, Salehe Mbega, alisema uwekezaji wenye thamani ya Sh bilioni 429.1 umewezesha kuongezeka kwa idadi ya meli zinazohudumiwa kutoka 100 hadi 616 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Mbega, uwekezaji huo pia umeongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena kutoka tani 400,000 hadi tani 2,170,000 kwa mwaka.
Ongezeko la meli na shehena limepanua shughuli zinazofanyika bandarini na hivyo kuongeza fursa kwa wananchi katika sekta mbalimbali zinazohusiana na huduma za bandari, biashara na usafirishaji.
Mbega alisema hali hiyo pia imeendelea kukuza mnyororo wa thamani unaozunguka Bandari ya Tanga, na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Mkoa wa Tanga na taifa kwa ujumla.

Leave a comment