
Na Grace Mwakalinga
Wananchi wa Buza, Dar es Salaam, wameilalamikia Serikali kuhusu changamoto za usafiri na utupaji wa taka, wakisema baadhi ya daladala hukatisha safari na kuwaacha njiani, huku kukosekana kwa maeneo maalumu ya kutupa taka kukichangia uchafu katika eneo hilo.
Malalamiko hayo yalitolewa jana wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipofanya ziara katika Soko la Tandika na Buza, ambako alikutana na wananchi na wafanyabiashara kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Wananchi hao walieleza kuwa changamoto ya usafiri imekuwa ikiwalazimu baadhi yao kushuka kabla ya kufika wanakokwenda baada ya madereva wa daladala kukatisha safari.
Aidha, walilalamikia ukosefu wa maeneo maalumu ya kutupa taka, wakisema hali hiyo inaweza kuathiri usafi wa mazingira katika eneo hilo.
Chalamila aliwataka wafanyabiashara wa Soko la Buza kuzingatia usafi na kutunza mazingira ili kuboresha hali ya soko na mazingira ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, wafanyabiashara walioondolewa katika maeneo yasiyo rasmi ya biashara Tandika pia walilalamikia kuuziwa meza kwa Shiliongi laki mbili (200,000) baada ya kuhamishiwa katika Soko la Buza.
Wafanyabiashara hao walimweleza Chalamila kuwa gharama hiyo imekuwa changamoto kwao wakati wakijaribu kurejesha shughuli zao katika eneo jipya waliloelekezwa na Serikali.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Jomali Satula, alisema hana taarifa kuhusu bei hiyo, akieleza kuwa shirikisho la wafanyabiashara ndilo lililofanya mazungumzo na mkandarasi na kufikia makubaliano ya Sh200,000 kwa meza.
Chalamila aliwataka wahusika kukaa pamoja na kutafuta suluhu ya changamoto hiyo, akisisitiza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kupewa mazingira yatakayowawezesha kuendelea na shughuli zao kwa utaratibu.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara walioondolewa Tandika kutumia Soko la Buza lililoandaliwa kwa ajili yao, badala ya kurejea kufanya biashara barabarani au katika maeneo yasiyo rasmi.
Alisema hatua ya kuwaondoa wafanyabiashara barabarani inalenga kuhakikisha njia zinakuwa wazi kwa matumizi ya wananchi na kuboresha mpangilio wa shughuli za biashara jijini.
Chalamila alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuingia katika mfumo rasmi, kutambulika na kulipa kodi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya nchi.
“Biashara zinatakiwa kufanywa kwa utaratibu. Tukifuga biashara za ujanja ujanja tutakosa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kuendelea kuwasaidia kupata maeneo rasmi ya biashara, wakieleza kuwa kuondolewa katika maeneo yao ya awali kumeathiri shughuli zao.
Kwa upande mwingine, Chalamila alisema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu katika maeneo hayo, ikiwemo uwekaji wa lami na taa, akieleza kuwa baada ya mazingira kuwa bora kuna uwezekano wa kuanzisha masoko ya usiku.

Leave a comment