
Na Abel Mwakingwe
Wadau wa sheria na haki za watoto wameitaka Serikali kurekebisha Sheria ya Ndoa ili mtoto wa kike asiruhusiwe kuolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18, wakisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda haki, ustawi na mustakabali wa mtoto.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), uliolenga kujadili changamoto zinazozuia marekebisho ya sheria hiyo na kutafuta njia za kuzitatua.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Wakili Tike Mwambipile, alisema Sheria ya Ndoa ina vipengele vinavyohitaji kufanyiwa mapitio, huku suala la ndoa za utotoni likiwa miongoni mwa maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele.

Alisema mtoto mwenye umri wa miaka 14 au 15 bado yuko katika hatua za ukuaji na anakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimwili, kihisia na kijamii, hivyo hawezi kutarajiwa kuwa tayari kubeba majukumu yanayoambatana na maisha ya ndoa.
Kwa upande wake, Meneja wa Programu kutoka Jukwaa la Haki za Mtoto Tanzania, Rogasian Massue, alisema wadau wanataka kuona mabadiliko ya sheria yatakayoweka miaka 18 kuwa umri wa msingi wa ndoa kwa mtoto wa kike.
Massue alisema takribani sheria sita zinazomhusu mtoto wa kike zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili ziendane na mahitaji ya sasa katika kulinda haki na ustawi wa watoto.
Alisema Serikali inapaswa kuendelea kulitazama suala hilo kwa upana, akieleza kuwa sehemu kubwa ya wadau na jamii inaunga mkono mtoto wa kike kuwa na haki ya kuingia katika ndoa baada ya kutimiza miaka 18.
Mjadala huo pia uliangazia namna ya kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyoruhusu ndoa za watoto na kuimarisha ulinzi wa mtoto wa kike dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuingia katika ndoa akiwa katika umri mdogo.
Wadau hao wameendelea kusisitiza umuhimu wa kurekebisha sheria ili mfumo wa kisheria uendane na jitihada za kulinda haki, usalama na ustawi wa watoto nchini.

Leave a comment