Na Grace Mwakalinga

VIJANA wa kikundi cha Msimamo Youth Educators wametumia michezo kuhamasisha usafi, afya na utunzaji wa mazingira, baada ya kuandaa shughuli iliyowakutanisha vijana katika michezo mbalimbali huku wakifanya usafi katika maeneo yanayozunguka Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Vijana hao walifanya shughuli hiyo katika Uwanja wa Mnyamani, Buguruni, jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani. Shughuli hiyo ililenga kuwaunganisha vijana na wadau wa mazingira pamoja na jamii, ambapo pamoja na kushiriki michezo, walifanya usafi na kupata elimu kuhusu madhara ya uchafuzi wa mazingira.

Michezo iliyochezwa ni mpira wa miguu na rede, huku washiriki wakielekezwa namna michezo inavyoweza kutumika kujenga afya, nidhamu na ushirikiano, pamoja na kuwahamasisha vijana kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa jamii.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Omary Mandari kutoka Msimamo Youth Educators, alisema wameamua kutumia michezo kama njia rahisi ya kuwafikia vijana na kuwahamasisha kushiriki katika utunzaji wa mazingira.

Alisema kupitia michezo, vijana wanaweza kufikisha ujumbe kuhusu utunzaji wa mazingira kwa wenzao na jamii kwa njia inayowavutia, huku wakitumia vipaji vyao kujenga afya na kutengeneza fursa za maendeleo.

Kwa mujibu wa Mandari, utupaji holela wa taka, hasa taka za plastiki, unaweza kuziba mifereji na njia za maji na kuongeza hatari ya mafuriko wakati wa mvua.

Katika shughuli hiyo, timu zilizofanya vizuri zilitunukiwa zawadi, huku washiriki wakihimizwa kuendelea kutumia michezo kama sehemu ya kujenga afya na kukuza vipaji.

Aidha, vijana na watoto wa kike walipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kushiriki katika michezo, ubunifu na ujasiriamali ili waweze kutumia vipaji vyao kujenga fursa za kiuchumi.

Mdau wa michezo kutoka Buguruni, Mbaraka Mwinyi, alisema kuunganisha michezo na elimu ya mazingira ni muhimu kwa sababu kunawafanya vijana kujifunza huku wakishiriki shughuli wanazozipenda.

Alisema michezo inaweza pia kutumika kuwaelimisha vijana kuhusu maandalizi dhidi ya athari za mvua kubwa na El Niño, ikiwemo umuhimu wa kutunza mifereji na njia za maji.

Kiongozi wa Taasisi ya Hope Haven, Huba Heri, na Mwanahamis Halfan wa TWECO, walisema ushiriki wa vijana katika shughuli za utunzaji wa mazingira kupitia michezo ni hatua muhimu kwa sababu unaweza kuwahamasisha vijana wengine kushiriki katika masuala ya mazingira na maendeleo ya jamii.

Mwanahamis alisema tukio hilo limeonyesha kuwa michezo inaweza kuwa zaidi ya burudani na mashindano, kwa kutumika kama jukwaa la kuwaunganisha vijana, kujenga afya na nidhamu, kukuza vipaji na wakati huo huo kuhamasisha jamii kutunza mazingira.

Posted in

Leave a comment