
Na Andrea Mlwafu
WANANCHI wanaoishi katika vijiji vyenye misitu ya hifadhi wameanza kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na biashara ya kaboni, huku mapato hayo yakisaidia kugharamia shughuli za maendeleo ya jamii na kuimarisha uhifadhi wa misitu.
Akizungumzia uzoefu wa Wilaya ya Tanganyika, Afisa Misitu wa Halmashauri hiyo, Bruno Mwaisaka, amesema wilaya hiyo imepokea zaidi ya Shilingi bilioni 34 kutokana na biashara ya kaboni.
Kwa mujibu wa Mwaisaka, mapato hayo yamechangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii, ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya, pamoja na kutoa ajira za muda kwa wananchi.
Mafanikio hayo yameelezwa katika mafunzo yaliyowakutanisha maafisa na wananchi kutoka maeneo ya Tanganyika, Mbulu, Mvomero, Mwanga na Korogwe, yaliyolenga kuwawezesha jamii kuelewa namna ya kushiriki na kunufaika na biashara ya kaboni.
Mafunzo hayo yamefanyika kupitia Mradi wa Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya Uwezeshaji Kifedha katika Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania, unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Washiriki wa mafunzo hayo walitoka katika vijiji ambavyo tayari vinanufaika na biashara ya kaboni pamoja na vile ambavyo bado havijaanza kupata mapato hayo, ili kujifunza vigezo na taratibu zinazohitajika katika kushiriki katika biashara hiyo.
Mwananchi kutoka Mvomero, Mwanangao Msanya, amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa kuhusu vigezo na taratibu zinazohitajika ili vijiji vinavyohifadhi misitu viweze kushiriki na kunufaika na biashara ya kaboni.
Kwa upande wake, Afisa Misitu Mwandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Siima Bakengesa, amesema mafunzo hayo yana umuhimu katika kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji.

Amesema ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi wa misitu ni muhimu katika kuhakikisha uhifadhi unakuwa na manufaa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye rasilimali hizo.
Mtafiti Kiongozi wa mradi huo, Dkt. Kajenje Nkukurah, amesema SUA inalenga kuwasaidia wananchi wa vijiji ambavyo bado havijaingia katika biashara ya kaboni kufanya maamuzi sahihi kuhusu ushiriki wao, pamoja na kuimarisha utawala na usimamizi wa mapato yanayotokana na biashara hiyo.
Amesema mapato hayo yanaweza kusaidia katika usimamizi endelevu wa misitu na kuchochea maendeleo katika jamii zinazoshiriki katika uhifadhi.
Mradi huo wa miaka mitatu unaongozwa na SUA kwa kushirikiana na NCMC na Chuo Kikuu cha Bangor cha Uingereza, ukiwa na lengo la kutathmini mapato ya kaboni kama njia ya kuwezesha kifedha uhifadhi na usimamizi wa misitu ya jamii nchini.

Leave a comment