Na Abel Mwakingwe

SERIKALI imeanza kuhakikisha watu wenye ulemavu, hususan wasioona, wanapata taarifa za tahadhari na maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza kuathiri maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba mwaka huu.

Hatua hiyo imechukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Kitengo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu, kwa kuandaa vipeperushi vya Nukta Nundu (Braille) vyenye maelekezo kuhusu hatua za kuchukua kabla na wakati wa mvua hizo.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha ujumbe wa tahadhari unawafikia wananchi wote bila kujali mahitaji yao.

Nderiananga alitoa kauli hiyo hivi karibuni jijini Dodoma, alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Chama cha Wasioona Mkoa wa Dodoma pamoja na wanahabari kwa ajili ya kuhakiki usahihi na ufasaha wa maudhui yaliyowekwa kwenye vipeperushi hivyo.

Amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha taarifa kuhusu majanga, tahadhari na namna ya kujikinga zinapatikana katika mifumo inayoweza kufikiwa na makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo watu wenye ulemavu.

Kwa upande wao, SHIVYAWATA na wawakilishi wa watu wasioona walishiriki katika mchakato wa kuhakiki maudhui ya vipeperushi hivyo, hatua inayolenga kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinaeleweka na zinaendana na mahitaji ya watu wenye ulemavu wa kuona.

Mvua za El Niño zinatarajiwa kuanza kuathiri maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba 2026, huku Serikali ikiwa imeweka mpango wa maandalizi na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa maelekezo kwa taasisi na mamlaka mbalimbali kutambua maeneo hatarishi na kuchukua hatua za mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.

Posted in

Leave a comment