• Na Andrea Mlwafu

    Serikali imeimarisha mkakati wa kuwashirikisha wasanii, waigizaji, wanamichezo na watengeneza maudhui katika kutoa elimu kwa umma kuhusu historia, chimbuko na misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hususan kwa vijana.

    Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema hayo leo, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa kikao kati ya ofisi hiyo na wadau hao kilicholenga kujadili mpango wa kutoa elimu ya Muungano kwa umma.

    Amesema wasanii na watengenezaji wa maudhui wana uwezo mkubwa wa kuhamasisha jamii kupitia majukwaa yao, ikiwemo mitandao ya kijamii na kwamba ushiriki wao utasaidia kuifikisha elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

    Alisema elimu ya Muungano ni ajenda ya kudumu inayolenga kukuza uelewa wa Watanzania kuhusu historia yao, walikotoka, walipo na wanakoelekea kama taifa na kusisitiza umuhimu wa kutumia vipaji vya wasanii katika kuimarisha na kuenzi misingi ya Muungano.

    Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Muungano katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, alisema kuwashirikisha wasanii na watengenezaji wa maudhui kutoka pande zote mbili za Muungano ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.

    Katika kikao hicho, mwimbaji wa taarab Hadija Omary Kopa na wadau wengine wamepongeza mpango huo na kueleza utayari wao wa kutumia akaunti zao za mitandao ya kijamii kutoa elimu kuhusu Muungano, hususan kwa vijana wanaowafuatilia.

    Wadau hao pia wamependekeza wanamuziki kuandaa nyimbo maalumu za kuhamasisha uzalendo na kuenzi Muungano, sambamba na kuimarisha utoaji wa elimu hiyo katika taasisi za elimu, kuanzia shule za msingi hadi vyuo.

    Wakirejelea takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wadau hao wamesema kuwa asilimia 77.3 ya Watanzania walizaliwa baada ya kuasisiwa kwa Muungano, hivyo kufanya elimu kuhusu historia na misingi yake kuwa muhimu kwa vizazi hivyo.

    Kikao hicho cha siku moja kimewashirikisha wasanii, waigizaji na watengeneza maudhui, wakiwemo Victor Victor, maarufu Nanga; Mohamed Mwinchande, maarufu Matofali; Ester Luckson, maarufu Mama Chanja; Amani Nzala Nzala; Vicent Njau, maarufu Kiredio; Fredrick Bundala, maarufu Sky Walker; na John Rojas, maarufu Simple the Boy.

  • Na Mwandishi Wetu

    Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imepanga kufunga kamera za CCTV katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti upotevu wa fedha, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato.

    Hatua hiyo pia inalenga kuzingatia uadilifu na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato ya halmashauri hiyo.

    Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ramadhan Kimara, wakati akizungumza na wakusanya mapato katika kikao kilichofanyika hivi karibuni katika ofisi za halmashauri hiyo.

    Kimara alisema uwepo wa kamera hizo utasaidia kuimarisha usimamizi wa mapato na kurahisisha shughuli za wakusanya mapato.

    “Tutafunga kamera katika maeneo yote, lakini tutaanza na Kituo cha Mabasi Kibiti na vituo vya ukaguzi vya Jaribu na Kibiti. Lengo letu ni kudhibiti upotevu wa mapato,” alisema Kimara.

    Aidha, aliahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wakusanya mapato, hususan upungufu wa vitendea kazi, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

    Aliwahimiza wakusanya mapato kushirikiana na kusimamia ipasavyo fedha zinazokusanywa, akisisitiza kuwa mapato hayo yanapaswa kuchangia uboreshaji wa huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Kibiti.

    Uamuzi wa kufunga kamera za CCTV katika maeneo ya vyanzo vya mapato ni sehemu ya juhudi za halmashauri hiyo za kudhibiti upotevu wa fedha, kuongeza makusanyo na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana zinatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

  • Na Happy Milion

    Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 22, anayedaiwa kumuua baba yake mkubwa kwa kumjeruhi kichwani kwa panga, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi katika eneo la Hongoro, Kibamba, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Jumanne Mlilo, tukio hilo lilitokea Oktoba 18, 2026, katika eneo la Mungu Mwema, Hongoro.

    Taarifa hiyo imeeleza kuwa Humphrey Elisamon, maarufu kwa jina la Msoka, mwenye umri wa miaka 63 na mkazi wa Hongoro, aliuawa baada ya kudaiwa kushambuliwa kwa panga kichwani na Dickson Elimringi Msoka, mwenye umri wa miaka 22, ambaye ni mtoto wa mdogo wake.

    Baada ya tukio hilo, Dickson alishambuliwa na wananchi kabla ya polisi kufika eneo la tukio. Polisi walimkuta akiwa katika hali mbaya, na alifariki dunia alipokuwa akipelekwa hospitalini.

    Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea.

    Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewataka wananchi kutumia njia za kisheria na kushirikiana na mamlaka husika katika kutatua changamoto zinazowakabili, badala ya kujichukulia sheria mkononi.

    Aidha, jeshi hilo limeeleza kuwa linaendelea na kampeni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kukutana na wananchi katika maeneo yao ili kubaini changamoto za kiuhalifu na kutafuta suluhisho.

    Wananchi wamehimizwa kushiriki kampeni hiyo wanapofikiwa na makamanda wao.

  • Na Mwandishi Wetu

    Wananchi 268 wamefanyiwa upasuaji wa macho bure, huku wengine 1,345 wakipatiwa miwani ya kusomea bila malipo katika Kituo cha Afya Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, kupitia kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya macho iliyolenga kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

    Kambi hiyo iliyoandaliwa na Lions Club DSM Host kwa kushirikiana na Majey Foundation, pia imewezesha wagonjwa 2,338 kupata huduma za matibabu ya macho kwa njia ya wagonjwa wa nje, pamoja na huduma za uchunguzi na dawa.

    Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Majey Foundation, Dk. Majala Majala, alisema huduma hizo zilitolewa bure kwa siku tatu na kambi hiyo ilihitimishwa Oktoba 18, 2026.

    “Tumekuwa na huduma za uchunguzi wa macho, ugawaji wa dawa na miwani, pamoja na upasuaji bure. Tumeshafanya upasuaji wa wagonjwa 268, tumegawa miwani 1,345 na kwa wagonjwa wa nje tumewahudumia 2,338,” alisema Dk. Majala.

    Alisema taasisi hizo zimekuwa zikiendesha kambi za aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwasaidia wananchi wenye changamoto za macho kupata uchunguzi na matibabu bila kikwazo cha gharama.

    Aliongeza kuwa baada ya kumaliza huduma Rufiji, wanatarajia kuelekea Simiyu, Chanika na Mwanza kwa ajili ya kuendesha kambi nyingine, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kupata vipimo na matibabu pindi wanapopata taarifa za huduma hizo.

    Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Ikwiriri, Dk. Jumanne Mapande, alishukuru waandaaji wa kambi hiyo kwa kuwasaidia wananchi waliokuwa na uhitaji wa huduma za matibabu ya macho.

    Alisema baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakishindwa kupata huduma za madaktari bingwa katika hospitali kubwa kutokana na changamoto za kifedha, hivyo kambi hiyo imewapa fursa ya kupata huduma walizokuwa wakizihitaji bila malipo.

    Dk. Mapande aliomba kambi hizo ziwe zinafanyika mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini ambao wanakabiliwa na changamoto ya gharama za kufuata huduma za kibingwa.

    Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hizo walieleza kufurahishwa na uwepo wa kambi hiyo kwa kuwa imewawezesha kupata matibabu karibu na makazi yao bila gharama.

    Kasimu Yassini, mmoja wa wagonjwa waliopata huduma, aliishukuru Serikali kwa kuunga mkono juhudi za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

    Naye Yusra Mitume, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Samia Suluhu Hassan, alisema kambi hiyo imemsaidia kupata dawa za macho kwa ajili ya kutibu changamoto iliyokuwa ikimsumbua kwa muda mrefu.

  • Na Majura Mathias, GAIRO

    Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Lukungu, wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 528, umefikia hatua ya upauaji, hatua inayotoa matumaini ya kuboresha upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa Kata ya Ukwamani, Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro.

    Mradi huo unafadhiliwa na Serikali Kuu kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), ukiwa na lengo la kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

    Kukamilika kwa shule hiyo kunatarajiwa kupunguza adha ya wanafunzi wa Kijiji cha Lukungu na vijiji jirani ambao hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda Shule ya Sekondari Sekwao kupata elimu. Aidha, shule hiyo inatarajiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Sekwao.

    Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliyotolewa hivi karibuni na Mwalimu Tabitha Mallo wa Shule ya Msingi Lukungu, miundombinu inayojengwa inajumuisha vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, matundu 11 ya vyoo, kichomea taka na jengo la maktaba.

    Miundombinu mingine ni jengo lenye maabara za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Baiolojia na Kemia, zitakazowawezesha wanafunzi kupata maarifa ya kinadharia na kufanya majaribio kwa vitendo.

    Mradi huo unalenga kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya sekondari, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora karibu na makazi yao.

    Ujenzi wa shule hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu na kupanua fursa za wanafunzi kupata elimu ya sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.

  • Na Happy Milion

    Mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 13 amefariki dunia, huku watu wengine 41 wakilazwa hospitalini baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu katika Kijiji cha Unyambwa, Manispaa ya Singida.

    Tukio hilo lilitokea Oktoba 17, 2026, baada ya washiriki wa shughuli moja ya nyumbani kula chakula aina ya makande na kunywa kinywaji aina ya togwa, vinavyodaiwa kuwa chanzo cha kuugua kwao.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto, waathirika walianza kuugua asubuhi ya Oktoba 18, 2026, wakilalamikia maumivu ya tumbo na kichefuchefu, hali iliyosababisha baadhi yao kupelekwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

    Taarifa hiyo ilieleza kuwa mtoto Ridhwani Omari alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Zahanati ya Moyo wa Yesu, Mangumitungo na mwili wake ulihifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    Aidha, watu wengine 40 walipelekwa katika Hospitali ya Manispaa ya Singida kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

    Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linawashikilia watu wawili, wakazi wa Kiji na Kata ya Unyambwa, kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.

    Jeshi la Polisi limewataka wananchi wa Unyambwa kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha tukio hilo na wahusika. Aidha, limeeleza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika kwa mujibu wa sheria.

    Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha tukio hilo, huku ikisubiriwa taarifa zaidi kutoka kwa mamlaka husika.

  • Na Happy Milion

    Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Abubakar Kunenge, amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kanda ya Kusini, Usharika wa Chabu, Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe.

    Akizungumza jana katika harambee hiyo, Kunenge alisema kuwa Waziri Mkuu alitarajia kushiriki katika shughuli hiyo baada ya kupokea na kukubali mwaliko, lakini alishindwa kuhudhuria kutokana na majukumu ya kitaifa na hivyo kumtuma Mkuu wa Mkoa kumwakilisha.

    Alieleza kuwa Waziri Mkuu ameahidi kuchangia shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.

    Kwa upande wake, Kunenge aliahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji. Aidha, alizitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ileje na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kuchangia mifuko 50 ya saruji kila moja ili kusaidia waumini kukamilisha ujenzi huo.

    Akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Augustino Senga, alisema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali na viongozi wa dini ni muhimu katika kudumisha amani na usalama wa wananchi.

    Senga alieleza kuwa mafundisho ya dini yanayohimiza maadili mema, kumcha Mungu na kujiepusha na vitendo vya uhalifu yana mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye amani na utulivu.

    Alisisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia mafundisho hayo na kuyatekeleza katika maisha yao ya kila siku ili kuimarisha usalama na kuwezesha shughuli za maendeleo kufanyika katika mazingira salama.

  • Na Yusra Temba

    UWANJA wa golf wenye mashimo 18, uliojengwa katika eneo la ekari 450 la Hifadhi ya Taifa Serengeti, umezinduliwa katika eneo la Fort Ikoma, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara, ukiwa na upekee wa kutokuwa na uzio ili kuruhusu wanyamapori kuendelea kutumia eneo hilo kwa uhuru.

    Uwanja huo wenye jumla ya Par 72 unatarajiwa kupanua wigo wa utalii wa michezo nchini na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa, kwa kuunganisha mchezo wa golf na uzoefu wa kutazama wanyamapori katika mazingira yao ya asili.

    Akizindua uwanja huo jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema Serikali inaendelea kubuni bidhaa mpya za utalii ili kuongeza mvuto wa nchi kwa wageni wa ndani na nje.

    “Serikali imeendelea kuweka mkazo katika ubunifu wa mazao mapya ya utalii yatakayoongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa,” alisema.

    Aliongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa wanyamapori na michezo barani Afrika.

    Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa, alisema uwanja huo unalenga kuongeza thamani ya vivutio vya nchi na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi, zikiwemo ajira, biashara na utoaji wa huduma katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.

    Uwanja huo pia umewekewa mfumo wa umwagiliaji wa maji ardhini unaolenga kusaidia utunzaji wa eneo la mchezo na kupunguza athari kwa mazingira, huku shughuli zake zikizingatia taratibu za uhifadhi.

    Naye Robinson Owiti, mchezaji wa kulipwa wa golf kutoka Kenya, alisema amefurahishwa na fursa ya kucheza katika uwanja huo, akieleza kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kutembelea Serengeti na kushuhudia wanyamapori katika makazi yao ya asili.

    Uzinduzi huo ulipambwa na burudani mbalimbali, zikiwemo ngoma za asili na muziki.

    Uwanja huo unaongeza aina ya shughuli zinazoweza kuvutia watalii Serengeti, huku ukitoa fursa ya kukuza utalii wa michezo sambamba na kuendeleza uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

  • Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi

    MNADA wa kwanza wa korosho wa msimu huu uliofanywa na Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI umezalisha mauzo ya kilo 10,830,000 za korosho zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 36, huku bei ya juu ikifikia Shilingi 3,410 kwa kilo na bei ya chini ikiwa Shilingi 3,270.

    Matokeo hayo yaliyopatikana jana katika makao makuu ya RUNALI wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, yameweka mwanzo wenye matumaini kwa msimu huu wa korosho, huku wakulima wakieleza kuridhishwa na bei zilizopatikana, wakizitaja kuwa nzuri ikilinganishwa na msimu uliopita.

    Akizungumza katika mnada huo akiwa mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, aliipongeza Serikali kwa juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo, huku akiwataka wakulima na wadau wa korosho kuongeza uzalishaji ili kufikia lengo la tani 300,000.

    Malima alisema mapato yanayotokana na zao hilo yana mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya wananchi na kukuza uchumi kupitia shughuli za kilimo.

    Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, alisema wilaya hiyo inalenga kuzalisha korosho zenye ubora wa daraja la kwanza (Grade A), akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora katika hatua zote za uzalishaji na utunzaji wa zao hilo.

    Alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha sifa ya korosho za Nachingwea na kuongeza ushindani wake katika soko.

    Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, aliwahimiza wakulima kudumisha ubora wa korosho, kuzipeleka sokoni kwa wakati na kuzihifadhi katika mazingira yanayokidhi viwango vinavyotakiwa ili kupata bei nzuri.

    Pia alisisitiza umuhimu wa kukagua korosho zilizohifadhiwa maghalani na kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

    Mwenyekiti wa RUNALI, Odas Mpunga, aliwataka wakulima kupeleka korosho zao sokoni kwa wakati na kuzingatia taratibu za uuzaji ili kuhakikisha wananufaika ipasavyo na zao hilo.

    Mauzo hayo ya mnada wa kwanza yanaweka matarajio mapya kwa wakulima wa korosho mkoani Lindi, huku juhudi za kuongeza uzalishaji, kudumisha ubora na kuimarisha masoko zikitarajiwa kuwa muhimu katika kuongeza kipato cha wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

  • Na Andrea Mlwafu

    Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuweka mpango madhubuti wa usimamizi wa Dampo la Pugu Kinyamwezi ili kudhibiti athari za taka kwa afya za wananchi na mazingira.

    Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Pius Yanda, pamoja na wajumbe wengine wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika dampo hilo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

    Profesa Yanda amesema ni muhimu kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na dampo hilo wanalindwa dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mrundikano wa taka, moshi na harufu. Ameipendekeza Halmashauri kuweka uzio kuzunguka eneo hilo kama sehemu ya kuboresha usalama na usimamizi wake.

    Aidha, wajumbe wa kamati hiyo wamehimiza kufanyika kwa tathmini ya athari za kiafya zinazoweza kuwakabili wakazi wa maeneo jirani na dampo hilo, ili kubaini ukubwa wa changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo.

    Kamati pia imesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa ujenzi wa madampo katika maeneo mengine kulingana na mahitaji, pamoja na kuhakikisha wazabuni wanaopewa jukumu la kukusanya taka wanakuwa na vifaa, rasilimali na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

    Ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Septemba 18, 2026, kuhusu kuboresha usimamizi wa taka katika Dampo la Pugu Kinyamwezi.

    Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha usimamizi wa taka na kuhakikisha zinageuzwa kuwa fursa za kiuchumi.

    Kwagilwa amesisitiza umuhimu wa kumpata mwekezaji mwenye uwezo wa kusimamia shughuli za uchakataji wa taka katika dampo hilo, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza athari za kiafya na kimazingira kwa jamii inayolizunguka.

    Ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushirikiana kwa karibu na taasisi zinazohusika na usimamizi wa mazingira, ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuhakikisha dampo hilo linasimamiwa kwa kuzingatia misingi ya uendelevu na uhifadhi wa mazingira.

    Katika ziara hiyo, kamati pia ilitembelea eneo la Mto Ng’ombe, wilayani Kinondoni, ambako ilipongeza juhudi za kuboresha mazingira ya mto huo, zikiwemo kazi za ujenzi wa kingo katika baadhi ya maeneo kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira.